Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Nassoro Makilagi amefanya kikao na wadau wa Mazingira katika ukumbi wa Sokoine Butimba wilayani Nyamagana Jijini Mwanza, leo tarehe 29/9/2022.
Katika kikao hicho chenye kauli mbiu " Tunza Mazingira ,ng'arisha Nyamagana" Mhe. Makilagi ameeleza umuhimu wa kuyatunza mazingira na kuyaweka katika hali ya usafi na kwamba ukitunza mazingira , yatakutunza. "Nimewaiteni ninyi wadau wa mazingira ili kwa pamoja tuifanye Mwanza kuwa ya kijani na yenye kuvutia kwa kupanda miti na maua sehemu za milimani, kando kando ya barabara, kando ya ziwa, kwenye makazi ya watu na sehemu za bustani zilizo kufa tuzifufuwe na kubuni maeneo mengine ambayo pia yatapendezesha mji wetu." Amesema Mhe. Amina Makilagi.
Akifafanua zaidi Mkuu wa wilaya ya Nyamagana amesema kamati maalumu ya mazingira imeundwa ili kuhakikisha elimu inatolewa zaidi kwa wananchi kuhusu mazingira na hasa kuhamasisha zaidi juu ya kampeini ya upandaji miti ikiwemo miti ya matunda na kuitunza.
Aidha amesema " Ili zoezi hili likamilike na kufanikiwa zinahitajika jumla Tsh. Milioni 120 ambazo zitapatikana toka kwa wadau mbalimbali wa mazingira. kila mtaa utapewa miti 600 ya miparachichi na kila mwenyekiti ahakikishe inapandea na kutunzwa katika eneo lake.
Sambamba na hayo Mhe. Makilagi amewataka wenyeviti wa mitaa, watendaji, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa ustawi wa jamii na wadau wote wa mazingira kuwa vinara wa kampeini hii kwa kusisitiza usafi, upandaji miti, na utunzaji miti na maua kila mtu katika eneo lake.
Akikazia jambo hilo, amewataka mawakala wote wa usafi kuwa makini na suala la usafi hasa maeneo ya masoko na katika kaya za wananchi bila kuacha uchafu kwenye kaya za watu.
Naye Bwana Hamisi wakala wa huduma xa misitu Nyamagana, ambaye ni mdau mkubwa wa misitu ameeleza umuhimu wa kutunza miti na ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa kuchangia kutoa miti hasa ya kupanda maeneo ya barabarani aina ya miashoki.
Mhe. Amina Makilagi amesisitiza suala la ushirikiano kaitika kufanikisha suala la usafi na utunzaji mazingira na kuifanya Mwanza kuwa ya kuvutia si kwa wanamwanza tu, bali kwa Watanzania na wageni kwa ujumla.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.